MYDUKA ONLINE
WhatsApp

kipande cha pili

 

Sehemu ya 2: Siku ya Kukutana Tena

Siku iliyoanza kwa kahawa ya majani na mandazi ya jana iliishia kwa "DM" ya ajabu kwenye whatsap. "Chipsi-Mwananyamala guy 😂"  ndivyo ujumbe ulivyosomeka. Yasmin alikuwa amenitafuta! Nilitabasamu hadi sikio la kushoto likatoka nje ya uso. Nilipojibu kwa emoji ya viazi viwili na moyo, alijibu, "Kumbe moyo wako si barafu kweli, umeyeyuka na moto wa mafuta ya chipsi?"

Tukakubaliana kukutana tena lakini safari hii, si foleni ya chipsi. Nilitafuta sehemu ya staha: maktaba ya karibu. Kichekesho! Kwani nani anakutana na mrembo maktaba siku hizi? Lakini nilijua kama tutaendelea ,na nilitambua kuwa ni msichana asiyetaka mambo mengi, lazima tuchague mwanzo unaoeleweka. Nilitaka tuzungumze bila muziki wa ghetto wala kelele za boda boda.

Alikuja saa nane kamili mchana  dakika mbili kabla ya mimi. Yaani nikafikiri kama nimeachwa kwenye harusi. 

Mazungumzo yetu yalikuwa ya kipekee. Tulizungumzia ndoto, maisha, familia na namna dunia ya sasa inavyopotosha mapenzi kuwa kama bidhaa ya kutumika na kutupwa. Yasmin aliniambia, "Sijawahi kuwa na boyfriend... si kwa sababu sifai, bali kwa sababu sitaki kufunzwa na 'boy' bali kufahamika na mwanaume anayeogopa MwenyeziMungu."

"Mapenzi ya kweli hayawezi kuishi kwenye mwili tu  yanahitaji akili, maombi, na moyo safi usio na mchezo wa kuigiza."

Niligundua hapa si mchezo wa kawaida. Yasmin hakuwa 'bae' wa kupostiwa leo na kusahaulika kesho. Alikuwa somo, na mimi nilikuwa mwanafunzi niliyekosa darasa miaka mingi. Kwa mara ya kwanza, nilitamani kumheshimu msichana kabla ya kumpenda.