Sehemu ya 1: Mwanzo wa Ajabu
Sikuwa na mpango wa kupenda tena. Hapana. Moyo wangu ulikuwa kama sanduku la barafu ulioshiba maumivu, uliofungwa, na uliokataa kabisa kutikiswa na kelele za mapenzi. Nilikuwa nimeweka nadhiri ya "single forever" baada ya kupitia vilio vitatu vya mwaka mmoja, kila kimoja kikidhoofisha imani yangu kwa kile wanachoita "true love".
Lakini dunia huwa na vituko vyake. Usiku mmoja nikiwa kwenye foleni ya chipsi-mayai pale Mwananyamala, nikiwa nimetinga tracksuit ya zamani na flip flops, nikamuona dada mmoja hivi aliyetokea kunivutia ghafla. Niligeuka kwa haraka kama kamera ya CCTV ili kumuangalia vizuri, na macho yangu yakatua mojakwamoja kwa msichana mmoja aliyekuwa amevaa baibui jeusi akiwa ni mwenye kuvutia machoni mwangu na moyoni mwangu pia. Sijui kama ni mapepo au njaa, lakini moyo wangu ulianza kudunda kwa kasi kama ndengu kwenye chungu.Nikaanza kujichekesha nae akaanza kucheka pia.Ikabidi nimuulize
"Unacheka nini?" nikauliza kwa utani wa haraka haraka. Akajibu, "Naangalia jinsi watu wanavyopiga foleni kwa chipsi kama vile ni visa vya kusafiria kwenda Ulaya."
Nikacheka. Kicheko cha kweli. Mara ya kwanza kwa muda mrefu.
Alikuwa tofauti. Hakuwa na maringo ya 'Instagram Slay Queen', hakuwa na lugha ya 'baby boy' na 'cashapp me'. Alionekana kama msichana wa kawaida, lakini mwenye roho ya kipekee. Tulizungumza kwa dakika tano.Na nikalazimika kumfungulia kile kilichopo moyoni mwangu na yale niliyoyapitia sikumchelewesha kwa kuwa nilihisi kupagawa naye kutokana na alivyonivutia.Hakuwa mbinafsi alinielewa na ikabidi tubadilishane namba, nilizungumza naye muda mfupi lakini nilihisi kama tumetoka kuishi maisha manne pamoja.
"Mapenzi ya kweli si lelemama, lakini pia si vita. Ni safari ya pamoja – ambapo kila mmoja anaweka bidii bila kutegemea malipo ya mwili."
Yasmin hilo lilikuwa jina lake. Na jina hilo likaanza kuchora historia kwenye moyo wangu. Siku hiyo ilinibadilisha. Ilinitikisa. Ilinirudisha mahali ambapo nilijua mapenzi hayajafa ila tulikuwa tunayatafuta kwenye njia za mkato.