🚪 Kipande 4: Mlango Usiotarajiwa
Baada ya kukataa kazi ya haramu, Yusuph alikalia uvumi mzito. Watu wakasema, “Huyu kijana ni mbishi. Hatapiga hatua.” Lakini Yusuph aliendelea na kazi yake, akitengeneza viti, meza na kabati kwa uadilifu na ubora wa hali ya juu bila kujali kile ambacho kilikuwa kikizungumzwa juu yake.
Siku moja, alitembelewa na mgeni aliyekuwa mzee, mwenye suruali ya khaki na bastola iliyoning’inia pembeni mzee wa kijeshi aliyekuwa amestaafu. Alitazama kazi za Yusuph kwa makini, halafu akasema: “Kijana, samani zako zina roho. Ungekuwa Ujerumani ungeitwa mbunifu wa karne!”
Yusuph akatabasamu, akajibu: “Asante babu, lakini najivunia zaidi kuwa muumini wa kweli kuliko mbunifu maarufu.”
Mzee akacheka sana, kisha akamweleza kuwa ni mratibu wa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana waaminifu. Alimwalika Yusuph katika mradi mkubwa wa serikali unaosaidia vijana kujiajiri kupitia ufundi.
“Tutakufadhili, tutakutangaza, tutakupa ofisi na mashine za kisasa. Masharti ni kuwa msafi wa roho na mikono. Je, uko tayari?”
Yusuph alijibu haraka: “Kwa ruhusa ya Allah na kwa dua ya mama yangu niko tayari.”
“Baraka huja pale unapoendelea kuwa mwaminifu hata kama hakuna anayekuona.Endelea kuwa mwaminifu katika kila unachokifanya unajiweka karibu zaidi na baraka.”
Usiku ule, Yusuph alilia kwa shukrani. Aliinua mikono juu, akasema, “Ewe Mola, wewe ndiye Mpangaji wa njia zisizotarajiwa. Uliponijaribu sikukukimbia, sasa unanipa zaidi ya nilivyoomba.”
Lakini mafanikio huja na majaribu mapya… alikutana na wivu, fitina, na mashindano yasiyo ya haki. Je, ataweza kusimama tena?