🛤️ Kipande 8: Nafasi ya Maamuzi
Yusuph alipokea simu ya bosi wake msaidizi: “Tuna kikao cha dharura kesho. Ikiwa hautafika, nafasi yako itatolewa rasmi kwa mtu mwingine.” Alishtuka, macho yakamtoka. Hakutegemea mapigo hayo kwa haraka hivyo.
Akajisemea kimoyomoyo: “Ni kazi tu. Lakini hii kazi ndiyo tumaini la maisha yangu, na ya mama. Nikikosa, si tu kazi inapotea ndoto nzima inaweza kufa.”
Alizungumza na mama yake kwa sauti ya huzuni: “Mama, kuna kikao muhimu kesho. Naweza kwenda?” Mama akasema kwa tabasamu lililobeba hekima: “Nenda mwanangu. Hii siyo kunikimbia mimi, ni kutimiza wajibu wako. Maombi yangu yatatangulia mbele yako.Nenda salama na ninaamini kila kitu kitakaa sawa mwanangu kipenzi Allah akulinde na akuongoze katika safari yako inshaalaah”
Yusuph akajiandaa safari ya usiku. Alihitaji kufika alfajiri. Alinunua tiketi ya basi ya usiku, lakini... basi liliharibika njiani! Saa tano usiku bado wapo porini, hakuna mtandao, hakuna njia ya dharura. Watu wakaanza kulalamika, mmoja akatupa utani: “Nani alilaani hii gari hadi jeki nayo imekufa?”
Wakati wengine wanachukia hali, Yusuph alitulia, akatoa msahafu mdogo mfukoni, akaanza kusoma dua kwa utulivu. Mzee mmoja akaangalia akasema: “Kijana kama wewe, ninyi ndio mnaokoa kizazi hiki. Wengine wanatukana, wewe unasoma dua.”
“Maamuzi magumu huja kwa wale walio tayari kubeba majukumu makubwa.” Mara zote fanya maamuzi magumu kwa lengo la kubeba majukumu makubwa.
Asubuhi ilipokaribia, gari likawa tayari. Yusuph alifika jijini dakika 20 kabla ya kikao. Lakini alipofika ofisini, alikuta mlango umefungwa... na tangazo linalosema: "Kikao kimehamishiwa hoteli ya G-Luxury. Muda umeongezwa hadi saa 3:00 asubuhi."
Je, alitupwa nje au nafasi yake bado ipo? Alifika kwenye hoteli akiwa jasho linamtoka, lakini kitakachomsubiri mle ndani ni zaidi ya nafasi ya kazi... ni fursa ya maisha yake!