🌧 Kipande 6: Njia ya Mvua na Miiba
Baada ya kupokea barua ya vitisho, moyo wa Yusuph ulichanganyikiwa. Kwa mara ya kwanza tangu aanze kupambana, alihisi huzuni ya ndani iliyochanganyika na hofu. Hakujua kama kesho ingeisha salama.
Usiku huo, alijifungia kwenye chumba chake, akafungua Qur’an na kuanza kusoma suratul Yasin. Machozi yalimtoka taratibu. “Ewe Mola, nisamehe kwa yote, niongoze. Nikikosea, nielekeze. Nikidhoofika, nipe nguvu.”
Asubuhi ilipofika, aliamka akiwa na amani moyoni. Akaenda kazini kama kawaida lakini macho ya watu yalikuwa tofauti. Wengine walitabasamu, wengine walimkodolea macho ya chuki. Barua ya vitisho ilikuwa imesambazwa kwa wafanyakazi wenzake na mitandaoni!
Mwandishi mmoja wa gazeti mashuhuri alimfuata kwa lengo la kumchafua. “Tuna taarifa kwamba unatumia dini kama mbinu ya kupata umaarufu,” akasema kwa dharau. Lakini Yusuph alitabasamu tu: “Mimi sifanyi kwa sifa, nafanya kwa imani. Siku zote ukweli hauhitaji makelele kwahiyo sioni haja ya kupiga kelele kwa lengo la kutaka kujitetea la hasha.”
Watu wengi walivutiwa zaidi na ujasiri wake. Hata waliomsema, wakaanza kufikiri mara mbili. Simulizi ya Yusuph sasa ikawa gumzo sio tu kwa vijana, bali hata kwa viongozi kazini.
“Ukitaka kuwa taa, kubali kuungua. Mafanikio ya kweli yanatokana na kuvumilia miiba ya njiani na sio kwa kukata tamaa kirahisi.”
Lakini wakati hali ikiwa inaonekana kutulia, mama yake mzazi alianguka ghafla na kulazwa hospitali ya rufaa. Ndoto zake sasa zilikuwa katika mzani wa imani na majukumu ya kifamilia.
Je, atachagua kuendelea na kazi za kijamii au atarudi kijijini kumtunza mama? Safari yake bado ndefu…