MYDUKA ONLINE
WhatsApp

kipande cha saba

Sehemu ya 7: Duka la Hidaya

Yasmin alinitumia meseji isiyo ya kawaida: “Leo nakualika mahali spesho. Naitwa kazini Duka la Hidaya, utajifunza kitu.” Nilijua ni duka la Kiislamu, lakini moyo wangu ulichanganya imani na mapenzi kwa kasi ya 5G.

Nilipofika, nikakuta anahudumia wateja, akiwa amevaa khimar ya kijivu na apron yenye maandishi: “Huduma kwa Tabasamu”. Mteja mmoja alimwambia, “Wewe ni Yasmin wa nyota ya jannah au wa mapenzi ya halal?”
Yasmin akajibu kwa kicheko, “Mimi ni mfanyabiashara wa akhera, siyo wa hisia za muda mfupi.” 😄

Niliposogea, aliniambia, “Leo unajifunza kuuza vitabu vya dini na siyo kuuza maneno matamu mitandaoni.”
Nikajibu, “Usijali, nina lugha laini kuliko karatasi ya kitabu.”

Kabla sijaanza kazi, alinipa kijitabu kidogo: “Adabu za Mahusiano Halali.” Niliposoma ukurasa wa kwanza, nilikutana na maneno haya:

"Mapenzi ni ibada pale yanapozingatia mipaka, lakini ni majanga pale yanapovunja mipaka ya dini."

Duka likaanza kujaa. Nilimsaidia kupokea wateja, kuwasomea faida za mafuta ya mbarika na manukato ya Oud. Mzee mmoja akanishika mkono na kusema, “Kama wewe ni mchumba wa huyu binti, huna budi kuwa na sabr ya Nabii Ayoub!” 😂

Baada ya kazi, tukakaa nje ya duka chini ya kivuli cha mwarobaini. Yasmin akaniambia, “Leo umejifunza nini?”
Nikajibu, “Nimejifunza kuwa mapenzi siyo tu ujumbe wa kila dakika, bali ni kushirikiana katika mambo ya kheri.”

Akatabasamu kistaarabu, kisha akasema, “Mpenzi wa kweli si yule anayetaka picha yako kila siku, bali anayetaka uswali nawe kila siku.”

Nikanyamaza kimya kwa sekunde kumi, halafu nikasema, “Nataka tuwe washirika wa Duka la Hidaya  hapa duniani na kesho akhera.”

Tukacheka. Kicheko cha watu wawili waliogundua kuwa safari ya mapenzi ya kweli si mitaa ya mji bali njia ya kuelekea radhi za Mwenyezi Mungu.